Tuesday, March 6, 2012

profesa maji marefu chupuchupu kuporwa gari na majambazi mombo


Mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani 'almaarufu Profesa Majimarefu' akionesha sehemu ya kioo katika gari lake aina la lexus lenye namba za usajili T 265 BLS ambalo limevunjwa vioo na watu wanaohisiwa kuwa majambazi.
Na Ripota wetu, Tanga
MBUNGE wa jimbo la Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani ‘almaarufu Profesa Majimarefu’, usiku wa kuamkia leo alivamiwa na watu wanaohisiwa kuwa majambazi  katika eneo la Mombo, walipoweka mawe barabarani kwa lengo la kuteka magari.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini, Profesa Majimarefu alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 7:00 usiku wa kuamkia jana katika eneo hilo alipopita wakati akitokea Jijini Nairobi kuelekea Tanga kwenye mkutano wa wadau wa mkonge  uliofanyika jana kwenye ukumbi wa mkuu wa mkoa.
Akielezea tukio hilo, mbunge huyo alisema kuwa wakati alipofika eneo hilo walikuta mawe yamepangwa barabarani na dereva wake alipoona hali hiyo aliingia kwenye mtaro kuyakwepa mawe hayo lakini wakiwa pembeni ya barabara, walitupiwa mawe ambayo yaliweza kuvunja kioo cha gari upande aliokaa mbunge huyo.
“Tulipofika eneo hilo Hoteli ya Liverpool naiona ile pale, tukakuta mawe barabarani dereva wangu Omari kuyaona akaingia pembeni kuyakwepa kule pembeni tulitaka kupinduka, lakini majambazi wale waliturushia mawe yaliyovunja kioo,” alisema mbunge huyo huku akionesha gari hilo kwa waandishi wa habari.
Akielezea zaidi alisema alitoka Jijini Nairobi majira ya saa 12:00 jioni Jumapili kuelekea Jijini Tanga kwenye mkutano huo lakini alipofika katika eneo la Manga –Kibaoni akiwa anaendesha yeye gari hilo lenye namba T 265 BLS aliamua kuweka gari pembeni ili wapumzike kisha waendelee na safari.
“Tulilala pale kama dakika 20 hivi dereva wangu aliamka akasema mzee hatuwezi kulala hapa bora tusogee mbele maana tumeshafika Korogwe bora tukalale nyumbani kisha kesho (jana) twende Tanga mkutanoni, nilimkubalia kumbe tunakwenda ‘kwenye mtaji wa masikini’,” alisema mbunge huyo.
Mbunge huyo alisema tukio atahakikisha anashirikiana na wananchi wa eneo la Mombo kuhakikisha vijana wanaojihusisha na uhalifu na kuchafua sifa nzuri ya wakazi wema wa eneo hilo, wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa polisi mkoani Tanga, Constantine Masawe alikiri kutokea kwa tukio hilo ambaloaalisema kuwa jeshi hilo tayari limeanza kazi ya kuwasaka watu hao waliofanya uhalifu ili waweze kuwakamata kutokana na vitendo hivyo.

No comments:

Post a Comment