Picha na habari na Francis Dande
AZAM FC, leo imefanikiwa kukalia kilele cha Ligi Kuu ya Tanzania Bara, baada ya kuwafanyia ‘kitu mbaya’ mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga kwa kuwachapa mabao 3-1 katika pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mabao mawili, moja kila kipindi kutoka kwa mshambuliaji anayekosa makali avaapo jezi za taifa, John Bocco ‘Adebayor’ dakika za nne na 76, na lile la Balou Kipre dakika ya 54, yalitosha kuiweka Azam kileleni kwa kufikisha pointi 41, huku Simba ikishika nafasi ya pili kwa pointi 40 na Yanga kubaki nafasi ya tatu kwa pointi 37.
Bao la Bocco dakika ya nne, lilikuwa na mchango mkubwa katika kuichanganya Yanga, iliyoapa kumalizia kwa Azam hasira za kuchapwa na kutupwa nje katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek, na kuifanya ianze kutembeza ubabe dimbani hapo.
Baada ya bao hilo, Yanga ikaonekana dhahiri kuchanganyikiwa na athari ya hili ikaanza dakika ya 11, ambapo kiungo Haruna Niyonzima ‘Fabregas alionywa kwa kadi ya njano baada ya kukaidi agizo halali la mwamuzi, Israel Mujuni, kwa kupiga mpira wakati filimbi ilishapulizwa.
Dakika mbili baadaye, akapewa kadi ya njano ya pili kwa kulalamika na kubishana na mwamuzi aliyeamuru mpira upigwe kuelekea Yanga baada ya Mnyarwanda huyo kumchezea rafu beki wa Azam.
Ni kadi iliyobadili hali ya hewa uwanjani hapo, na pambano kusimama kwa dakika tisa huku ‘mapambano yasiyo ya ubingwa’ yakishika kasi.
Fujo zikaibuka dimbani hapo, huku wachezaji wa Yanga wakimtwanga ngumi mwamuzi, vurugu zilizozaa kadi nyekundu ya pili, safari hii akioneshwa Nadir Haroub ‘Cannavario’.
Licha kuendelea kwa pambano, maamuzi ya refa yakawa ya shaka kutokana na kutojiamini tena mchezoni.
Dakika ya 32, Hamisi Kiiza akaifungia Yanga bao lililokuwa la kusawazisha, akiitendea haki pasi ya beki Shedrack Nsajigwa ‘Fuso’.
Timu zikaenda mapumziko kwa sare ya bao 1-1, huku amani ikiwa bidhaa adimu ndani ya dimba kutokana na wachezaji wa Yanga kugeuza ulingo wa ngumi. Kipre akafunga la pili dakika ya 54, kabla ya Bocco kumaliza kazi dakika ya 76.
Vurugu ziliendelea hata baada ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi, ambapo polisi walitumia mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na nyenzo nyingine kuwatawanya mashabiki, huku waandishi wa habari nao wakizuiwa kuingia chumba cha mikutano baada ya kumalizika kwa mchezo.
Akina Ras Makunja wakimsindikiza mwamuzi wa mchezo kati ya Yanga na Azam, Israel Mujuni baada ya kutokea vurugu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mwamuzi msaidizi, Hamis Changwalu akitoa akijaribu kumzuia mshambuliaji wa Yanga Shamte Ally asimshambulie mwamuzi wa mchezo huo |
Wafanyakazi wa huduma ya kwanza wakimpeleka shabiki wa Yanga katika chumba cha kutoa huduma ya kwanza baada ya kuzimia Uwanjani. Kufungwa nomaaa!
Mshabiki akishughulikiwa na kina Ras Makunja
mashabiki wa azam
Mrisho Ngasa wa Azam akitafuta mbinu za kumtoka beki wa Yanga, Nadir Haroub 'Canavaro' wakati wa mchezo huo
Akina Ras Makunja kazini....
No comments:
Post a Comment