Nimeandika machache yafuatayo baada ya vishindo vinavyosikika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kuhusu gurupu au magurupu ya watu fulani kuingiziwa haki zao kwenye Katiba ya Tanzania.
Watanzania wenzangu, pamoja na viongozi wa siasa nchini, kwa nia njema na kwa faida yetu sote na vizazi vijavyo, nasisitiza tusije tukaingia kwenye mtego wa kuanza kubainisha na kuainisha makundi ya watu kuwa na haki kadhaa wa kadhaa ndani ya Katiba mpya ya Tanzania.
Makundi ya watu yako mengi na yana mahitaji mbalimbali, lakini hatuwezi kuyabainisha moja baada ya moja na kuyapa HAKI kwa kuandika mahitaji ya magurupu hayo au gurupu lolote linalopendekeza haki zao ziandikwe ndani ya katiba ya Tanzania, hiyo itakuwa si Katiba yetu adhimu, bali tutakuwa tunachapisha kitabu cha haki za binadamu.
Tukifanya hivyo, kila kundi na taasisi zao wataomba haki zao kubainishwa na kuainishwa kwenye Katiba, mfano wa makundi hayo ni kundi la Wanaume, Wanawake, Watoto, Wazee, Vilema wa macho, miguu, mikono, masikio n.k.
Ingawa makundi yote haya ni ya kibinadamu na wana haki zao za KIBANADAMU (bila ya kuvuka mipaka ya Utamaduni wa Kitanzania na mipaka ya Kidini yenye kumgusa kila Mwanadamu na jamii kwa ujumla), mbiyu yetu ya Tanzania inayosema ‘Binadamu wote ni sawa’, ni mbiyu ambayo tumeifuata, imetutosheleza na imeleta mifano dhahiri ya kimaendeleo ambayo ipo wazi na ya kuonekana.
Lakini, tukianza kubainisha magurupu ya watu kwenye Katiba, italeta utata wa kijamii na tukae mkao kula kubadilisha Katiba kila miaka kumi kuridhisha magurupu ya watu watakaotaka haki zao kuwemo kwenye katiba.
Tusipoangalia, yatakuja kuzuka makundi mengine kwenye uhai wetu au kizazi kijacho ambayo yataleta mparaganyiko wa kijamii ambayo yataombelewa haki zao kuwamo kwenye Katiba na kuwacha taifa letu kwenye hali mbaya ya mipasuko na ghasia mitaani, kwa madai kuwa, ikiwa tumeweza kuandika gurupu fulani kwenye katiba, kwanini tusiandikiwe gurupu letu kwenye katiba hiyo na sisi ni Watanzania?
Nataraji sote tumefaidika na haya machache na samahani kama nimekosea na huu ni mchango wangu.
Ndugu yenu,
Saleh Jaber.
No comments:
Post a Comment