Saturday, March 17, 2012

Barwany Albinism Development Trust Fund (BADEF) Kupitia Kampeni ya Nifahamu Yaendelea Kukuza Ustawi wa Walemavu wa Ngozi Nchini

 Mbunge wa Lindi Mjini Salum Barwany akimkabidhi mafuta (lotion) Agneta Malawale kwa ajili ya kulinda ngozi dhidi ya mionzi ya jua wakati alipoenda kutoa msaada huo katika hospitali ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es salaam 

Mbunge wa Lindi Mjini Salum Barwany akimkabidhi sabuni muuguzi wa Hospitali ya Ocean Road Rose Ngowi kwa ajili ya kulinda ngozi dhidi ya mionzi ya jua kwa ajili ya walemavu wa ngozi(albino)wakati alipoenda kutoa msaada huo katika hospitali ya Ocean Road 

·         *BADEF yatembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dar es Salaam kupitia ushirikiano na sekta ya afya
      *Yazindua matembezi ya hisani yatakayofanyika 07/04/2012 kuchangisha fedha ili kuwawezesha  watu wenye ulemavu wa ngozi nchini

Taasisi isiyo ya kiserikali Barwany Albinism Development Trust Fund (BADEF), kupitia kampeni ya Nifahamu iliyozinduliwa Disemba mwaka jana yazidi kuimarisha ustawi wa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini. Mh. Salum Khalfan Barwany mwanzilishi na mwenyekiti wa BADEF leo pamoja na wadau alitembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road kupitia mpango na sekta ya afya kuimarisha maslahi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, na kutoa mafuta maalum yanayosaidia kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya ngozi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na pia kutoa vyakula kwa wagonjwa.

“Nikiwa miongoni mwa walemavu wa ngozi, nimeanzisha shirika lisilo la kiserekali (BADEF) linalohusika na kuleta ustawi kwenye maisha ya walemavu wa ngozi nchini.Mh. Barwany alisema. “kupitia Kampeni hii ya Nifahamu tunatoa ujumbe ufuatao:

a).Nilinde – Nina haki ya kuishi kama binadamu mwingine yeyote, pia nahitaji hifadhi ya maisha yangu.       

 b).Nijali – Ninastahili heshima, kuthaminiwa na kupewa huduma na mahitaji           maalumu
c).Nielimishe – Niwezeshe kujitambua, na kujilinda na jamii initambue na kunilinda
d).Naweza – Ninastahili kupewa fursa kama binadamu mwingine yeyote
e).Nipende – Mimi ni mwanadamu kama mwingine yeyote na ninastahili furaha, mapenzi na huruma.

Nawaomba watanzania wenzangu kuungana na mimi kwa kushiriki kwenye kampeni ya Nifahamu. Lengo kuu la kampeni hii ni kuelimisha jamii kuondokana na mtazamo hasi kwa walemavu wa ngozi nchini ambao umekuwa ukiendelea kwa miaka mingi sasa.

Mtazamo huu umechangia kuleta maafa mbalimbali kwa walemavu wa ngozi, kwa mfano: mauaji ya kikatili, kukatwa kwa viungo vyao na hivyo kuwaongezea ulemavu zaidi, kutengwa na kutohusishwa kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii,kiuchumi,kisiasa na kiutamaduni”. Aliongeza

Alizidi kusema,“Walemavu wa ngozi wanachangamoto nyingi sana katika jamii. Ukiachana na mtazamo hasi, wanakumbwa na majanga mengi yafuatayo: hatari ya ugonjwa wa saratani ya ngozi, imani potofu, uoni hafifu na jamii kuwa na  uelewa mdogo juu ya ulemavu wa ngozi.

Jamii ya watu wenye ulemavu wa ngozi inatengwa na kunyanyasika sana. BADEF, kwa kutambua hilo imeandaa matembezi ya hisani yenye lengo la kukusanya kiasi cha fedha cha Tsh. Milioni 500 kwa ajili ya kuchangia ili kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini kupitia njia zifuatazo:

a).Kufanya tafiti mbalimbali juu ya hali ya watu wenye ulemavu wa ngozi kv. Kielimu, kiafya na kijamii;
b).Kutoa elimu ya ulemavu wa ngozi;
c).Kuhamasisha ujumuishwaji kwenye sekta mbalimbali nchini na;
d).Kutoa vifaa vya kukinga

“Unaweza ukashiriki na kuunga mkono kampeni hii kwenye matembezi ya hisani yatakayofanyika tarehe 7/04/2012 saa kumi na mbili asubuhi. Matembezi haya yataanzia kwenye viwanja vya Leaders Club kinondoni mpaka viwanja vya Mnazi Mmoja .Vilevile unaweza kuchangia kupitia: Mpesa Namba; 0769696999, Airtel Money Namba; 0688858535, Tigo PesaNamba; 0655029595 au kwenye akaunti ya BADEF (CRDB Bank, Lumumba Branch Akaunti Na. 0150278228900).” Kufanikisha kampeni hii tunahitaji ushirikiano wa hali na mali kutoka kwa kila Mtanzania. Tunatumaini utaguswa na kujali kuungana nasi.”



Kwa maelezo zaidi kuhusu kampeni hii na matembezi ya hisani, ungana na wasiliana nasi kwenye mtandao kupitia:

Barua pepe: skbarwany@gmail.com,
Simu: 0713 690 637



Kwa mawasiliano:
Simu: 0686240279




No comments:

Post a Comment