Mgombea wa Chama Cha Sauti ya Umma (SAU) jimbo la Arumeru Mashariki, Shabani Kirita akihutubia katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake, leo kwenye viwanja vilivyopo eneo la Majani ya Chai jimboni humo.
Mgombea huyo akinadiwa na Mwenyekiti wa Jimbo wa chama hicho, Elias Matoto (kulia) katika mkutano huo wa uzinduzi wa kampeni za SAU kwenye viwanja vilivyopo eneo la Majani ya Chai jimboni Arumeru Mashariki. Kushoto ni Meneja wa kampeni za SAU Johnson Mwangozi
NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Sauti ya Umma (SAU) kimesema vyama vya upinzani hapa nchini vimekuwa vikishindwa na CCM katika uchaguzi mbalimbali kwa sababu ya ubinafsi.
Hayo yalisemwa leo na mgombea ubunge jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya chama hicho, Shabani Kirita wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika Majani ya Chai.
Alisema, njia madhubuti ambayo ingewezesha upinzani kuishinda CCM ni kwa vyama vya upinzani kuwa na kuungana, lakini akasema hilo limekuwa likishindikana kila unapotokea uchaguzi kutokana na uroho wa viongozi katika vyama hivyo hasa vyenye ruzuku.
Kirita alivitaja vyama vye kupata ruzuku kuwa ni pamoja na CUF, CHADEMA, UDP, NCCR Mageuzi na TLP, na kwamba viomgozi wa vyama hivyo ni walafi wa kupindukia ndiyo sababu hakuna hata mmoja kati yao anayefikiria kuwa ni muhimu vyama vya upinzani kuungana dhidi ya CCM.
"Sisi SAU tunasema kwamba tuna miaka michache katika ulingo wa siasa hapa nchini, lakini 'tunatisha' na kwa sababu tunaamini kwamba tupo kwa ajili ya kuinua maisha ya wananchi kwa kutumia sauti ya umma tupeni nafasi ya ubunge hapa Arumeru tuonyeshe mfano", alisema.
Alisema, wakati baadhi ya vyama vinajinadi kuwa ni 'Nguvu ya Umma' faida ya nguvu hiyo imekuwa ikiwanufaisha viongozi wa vyama hivyo wakati umma unaowaunga mkono ukiendelea kudorora kimaisha.
Kwa upande wake Meneja wa kampeni wa mgombea huyo, Johnson Mwangosi aliwataka wana Arumeru Mashariki, kuchagua mgombea mwenye sifa zitakazowanufaisha wote, na siyo kwa kulazimishwa au kutishwa na viongozi wa vyama vya wagombea.
Aliwataka vijana kujiepusha kutumiwa na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wagombea kama chambo cha kuwa mstari wa mbele kwenye vurugu kwa manufaa ya viongozi hao.
"vijana jihadharini sana, msitumbukie katika vujo na vurugu wakati wa kampeni na kwenye uchaguzi wenyewe kwa sababu eti umepewa bia mbili, ukiingia katika mtengo huo ukiumia, kufa au kukamatwa utakuwa peke yako", alisema.
Kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Arumeru mashariki zilianza kurindima tangu Machi tisa mwaka huu, na zitatia nanga Machi 31, mwaka huu kupisha uchaguzi utakaofanyika Aprili Mosi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment