Tuesday, March 20, 2012

rais wa zanzibar dr shein ashiriki MAZISHI YA ALIYEKUWA MWANASHERIA MKUU WA KWANZA WA ZANZIBAR Wolfgang Dourado



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akiweka shada la Mauwa katika kaburi la marehemu Wolfango Dourado,aliyekuwa Jaji Mkuu na mwanasheria mkuu Mstaafu wa Zanzibar,huko mwanakwerekwe mjini Zanzibar leo. Picha na Ramadhan Othman IKULU. 
=====   ======   ======



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohammed Shein leo ameshiriki katika Mazishi ya aliyekuwa Jaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 Wolfgang Dourado ambaye alifariki dunia jana katika hospitali ya Zanzibar Medical Group Vuga mjini Zanzibar.

Katika mazishi hayo ambayo yaliwashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd yalitanguliwa na Sala maalum ya kumuombea marehemu iliyofanyika katika Kanisa la Minara Miwili Shangani Mjini Zanzibar.

Akitoa Salamu za Rambi Rambi kwa niaba ya Serikali kufuatia kifo hicho Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais amesema kifo hicho kimeacha pengo kubwa kwa kumpoteza mtu ambaye alikuwa muhimu katika kutoa michango yake katika utayarishaji wa sheria na maamuzi ya kimahkama jambo ambalo halitasahaulika milele.

Amesema kifo hicho si cha wanafamilia pekeyao bali ni kwa taifa zima la Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutokana na mchango mkubwa ambao alikuwa akiutoa hata kabla ya awamu ya kwanza ya utawala hadi kilipomfika kifo chake.

Aidha Waziri Aboud ameiomba familia ya Marehemu  Dourado kuwa na subra katika kipindi hiki cha msiba na kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo bega kwa bega na wanafamilia hao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Marehemu Wolfgang Dourado alizaliwa Zanzibar Septembar 20 mwaka 1929 na kupata Elimu yake  katika Skuli iitwayo St. Joseph Convert ya Zanzibar katika mwaka 1939-1946

Mnamo Mwaka 1947-1950 Marehemu Dourado alianza kazi Serikalini kama Karani wa Ardhi ambapo mwaka 1952 alihamishiwa Afisi ya Mrajisi Mkuu wa Serikali na mwaka 1954 alipewa Cheo cha Msaidizi Mrajisi Mkuu.
Mwaka 1954-1957 alipelekwa Uengereza kwa masomo ya juu na aliporejea masomoni alishika nafasi mbalimbali za uongozi kama vile Permanent Hospital Home Affairs,External Affair and Trade  na hatimaye kuwa Mwanasheria Mkuu na Mrajisi Mkuu wa Zanzibar.

Nyadhifa nyengine alizowahi kuzishika ni Mwenyekiti wa Bodi ya Uhamiaji,Bodi ya Kodi na Bodi ya Bima Zanzibar na lakini pia katika Shirika la Bima Zanzibar Marehemu alikuwa Meneja Mkuu.

Mnamo mwaka 1983 Marehemu Dourado aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya kurekebisha Sheria na Mwaka 1996 akiwa tayari amestaafu katika Utumishi aliteuliwa pia na Rais kuwa Jaji wa Mahakama kuu ya Zanzibar na hatimaye kuwa Naibu Jaji Mkuu.

Aidha Marehemu aliwahi kukabiliana na kesi nzito nzito zikiwemo zile zilizohusu mapambano ya Juni 1961, kuuwawa kwa Marehemu Mzee Abeid Aman Karume 1972 na kushiriki kama Mjumbe wa Tume ya Rais inayoshughulikia mambo ya Siasa 1991.Marehemu Wolfgang Dourado ameacha Mjane


IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 20/03/2012

No comments:

Post a Comment