Saturday, March 17, 2012

Yanga yaifanyia kitu mbaya Villa Squad kwa kuichapa 1-0

 Kocha wa Yanga, Kostadin Papic akipeana mkono na waamuzi wa mchezo huo baada ya kumalizika kwa mchezo 
 Mshambuliaji wa Yanga Hamis Kiiza akimtoka beke wa Villa Squad
 Mshambuliaji wa Yanga, Hamis Kiiza akiwatoka mabeki wa Villa
Kocha wa Yanga, Kostadin Papic akipeana mkono na waamuzi wa mchezo huo baada ya kumalizika kwa mchezo.

Habari na Picha na Francis Dande
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Yanga, leo wamefanikiwa kupanda nafasi moja na kushika nafasi ya pili baada ya kuwashusha kwenye msimamo wa ligi hiyo Azam FC, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Villa Squad, katika pambano gumu lililochezwa kwenye neshno la Taifa jijini Dar es Salaam.

Bao la dakika ya 90 lililowekwa kimiani na mshambuliaji wa Kimataifa, Hamisi Kiiza kutoka Uganda, lililotokana na kazi ya ziada ya Pius Kisambale, lilitosha kuwapa pointi tatu muhimu, zinazodumisha mbanano dhidi ya vinara Simba, wanaoongoza ligi hiyo kwa pointi 44, moja dhidi ya Wanajangwani, ambao walishinda mechi iliyopita dhidi ya African Lyon kwa bao 1-0.

Hata hivyo, bao hilo liliendeleza wimbi la kuvurunda miongoni mwa waamuzi, kutokana na Oden Mbaga, kulifumbia macho tukio la kipa wa Villa, Daud Mwasongwe, kugongwa akiwa ameshaudaka mpira huo, hivyo kumponyoka na Kiiza kumalizia nyavuni.
Pambano lilianza kwa mashambulizi ya kila upande, ambapo Yanga ilikuwa ya kwanza kupoteza nafasi ya maana dakika ya 11, pale Shamte Ali alipokosa bao kwa krosi yake kudakwa na Mwasongwe wa Villa, kabla ya dakika ya 15 Haruna Niyonzima ‘Fabregas naye kushindwa kuitendea haki pasi ya Keneth Asamoah.

Villa ikajibu mashambulizi hayo kwa kusaka na hatimaye kupata nafasi nzuri, lakini Stamiry Mbande, aliyewatoka mabeki wa Yanga, akapaisha shuti lake.

Dakika ya 27, Mwape kama kawaida yake akaikosesha Yanga bao na mpira wake kupaa juu ya lango la Villa na hadi mwamuzi anapuliza kipenga cha mapumziko, matokeo yalikuwa sare ya 0-0.

Kipindi cha pili, licha ya mabadiliko ya kila upande, milango ya kila timu ilikuwa migumu kuruhusu nyavu zake kutikiswa, hadi bao la Kiiza lilipomaliza ukame huo.

Katika jitihada za kusaka matokeo hayo, Yanga iliwatoa kwa nyakati tofauti nyota wake kadhaa, ingawa haikuwa rahisi kwao kupata walichokuwa wakikisaka dimbani hapo.

Villa nayo haikuwa nyuma, kwani ilifanya mabadiliko kadhaa yalioonekana kama yangewapa pointi muhimu katika raundi hii ya lala salama, kabla ya Kiiza kufunga bao hilo.

Katika mfululizo wa ligi hiyo, mechi nyingine ilipigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, ambako wenyeji Coastl Union waliibuka na ushindi kama huo wa bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro, bao lililowekwa kimiani kwa mkwaju wa penalti na Said Swedi dakika ya 18.




No comments:

Post a Comment