SEMINA ELEKEZI COPA COCA-COLA MACHI 25
Semina elekezi kwa ajili ya mashindano ya Copa Coca-Cola 2012 itafanyika Machi 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo washiriki ni makatibu wakuu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa au wawakilishi wao ambao wanatakiwa kuwa na utambulisho rasmi.
Washiriki kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam wanatakiwa kuwasili Machi 24 mwaka huu na watapokelewa katika hoteli ya Itumbi iliyoko Magomeni-Mwembechai.
TFF itawagharamia washiriki kwa chakula, malazi na nauli za kuja Dar es Salaam na kurudi kwa usafiri wa basi au meli.
Michuano ya mwaka huu itaanza Machi 31 hadi Mei 5 katika ngazi ya wilaya. Usajili kwa ngazi ya mkoa utaanza Mei 6 hadi 15 wakati mashindano yake yatafanyika kuanzia Mei 16 hadi 25.
Usajili na maandalizi kwa michuano ya ngazi ya Taifa utaanza Mei 26 hadi Juni 7. Usajili wa timu za mikoa unatakiwa kuwasilishwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kati ya Juni 8 na 14 mwaka huu.
WANYARWANDA KUCHEZESHA SIMBA, ES SETIF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua waamuzi kutoka Rwanda kuchezesha mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania Kombe la Shirikisho kati ya Simba na ES Setif itakayochezwa Machi 25 mwaka huu.
Mwamuzi wa kati ni Hudu Munyemana wakati wasaidizi wake ni Felicien Kabanda, Theogene Ndagijimana na Edouard Bahizi. Kamishna wa mechi hiyo ni Felix Tangawarima kutoka Zimbabwe.
Mechi hiyo namba 45 itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Mechi ya marudiano ambayo ni namba 46 itachezwa Aprili 6 mwaka huu nchini Algeria.
Iwapo Simba itafanikiwa kusonga mbele itacheza mechi ya kwanza nyumbani Aprili 29 mwaka huu na mshindi kati ya El Ahly Shandy ya Sudan na Ferroviario de Maputo ya Msumbiji ambapo ya marudiano itachezwa kati ya Mei 11, 12 na 13 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment