Friday, March 16, 2012

MUDA WA KUWASILISHA MAJINA YA WANAOPENDEKEZWA KUWA WAJUMBE WA TUME YA KUKUSANYA NA KURATIBU MAONI KUHUSU MABADILIKO YA KATIBA WAONGEZWA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, leo, Ijumaa, Machi 16, 2012, ameongeza muda wa kuwasilisha majina ya wanaopendekezwa kuwa wajumbe wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba kwa muda wa siku saba.

Sasa siku ya mwisho kuwasilisha majina hayo itakuwa siku ya Ijumaa, Machi 23, 2012.

Ifuatayo ni taarifa kamili kuhusu uamuzi huo kama ilivyotolewa na Katibu Mkuu wa Kiongozi, Bwana Ombeni Y. Sefue:

Mheshimiwa Rais alitoa mwaliko kwa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, jumuiya za dini, asasi za kiraia, jamii, taasisi na makundi mengine ya watu wenye malengo yanayofanana, kuwasilisha orodha ya majina ya watu wanaopendekezwa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume iliyotajwa hapo juu. Tarehe ya mwisho ya kuwasilisha orodha ya majina hayo ilikuwa ni leo, tarehe 16 Machi, 2012.

Hata hivyo, Mheshimiwa Rais anahisi kwamba pamoja na idadi nzuri ya majina ambayo tayari yamewasilishwa, bado yapo mapendekezo ambayo yametumwa kwa njia mbalimbali lakini yamechelewa kuzifikia ofisi za Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Inawezekana pia kwamba kuna watu ambao walitumwa na taasisi zao kutoka mikoani kuwasilisha mapendekezo hayo kwa mkono ambao pengine bado hawajafika. Aidha, inawezekana kuwa yapo mapendekezo mengine ambayo yametumwa kwa njia ya Posta na ambayo bado yapo njiani.

Kwa kuzingatia yote haya na kwa uzito na umuhimu wa jambo lenyewe, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameamua kuongeza muda wa kupokea mapendekezo kwa siku saba zaidi hadi tarehe 23 Machi, 2012.

Kwa msingi huo, siku ya mwisho ya kuwasilisha orodha ya majina sasa itakuwa tarehe 23 Machi, 2012.

Kwa wale ambao walichelewa kuandaa mapendekezo yao, wanaweza bado kutumia fursa hii ya kuongezwa kwa muda kuwasilisha mapendekezo yao kwa njia za haraka kama vile: njia ya mkono, kutumia nukushi na barua pepe. Mapendekezo yanayoletwa kwa nukushi na barua pepe yafuatiwe mara moja na nakala halisi.

Kwa mujibu wa mwaliko uliotolewa na Mheshimiwa Rais wadau mbalimbali wanatakiwa kupendekeza majina ya watu wasiozidi watatu wanaokidhi sifa zilizotamkwa katika kifungu cha sita cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Sifa hizo ni:-

(a) Uzoefu katika kufanya mapitio ya Katiba na sifa za kitaaluma za wajumbe kwenye mambo ya Katiba, Sheria, Utawala, Uchumi, Fedha na Sayansi ya Jamii.

(b) Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na

(c) Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii.

Kama ilivyokuwa awali, mapendekezo ya majina ya wajumbe wa Tume ya Katiba yaletwe kwa:-

Katibu Mkuu Kiongozi,
Ikulu,
S.L.P. 9120,
DAR ES SALAAM.
Nukushi: +255 22 2 11 72 72
Barua pepe: chief@ikulu.go.tz

Au: 

 Katibu wa Baraza la Mapinduzi na
Katibu Mkuu Kiongozi,
Ofisi ya Rais,
S.L.P. 4224,
ZANZIBAR.
Nukushi: +255 24 2 23 37 88

Ikulu,
DAR ES SALAAM.
16 Machi, 2012
2

No comments:

Post a Comment